Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imeibuka kinara miongoni mwa Taasisi za Elimu katika Maonesho ya 32 ya Kilimo, Mifugo na Sherehe za Nanenane Kanda ya Kaskazini 2026, yaliyofungwa rasmi leo katika Viwanja vya Themi Njiro, Arusha.

Ushindi huo unaonesha mchango wa NM-AIST katika kuendeleza utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu wenye lengo la kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya kilimo na mifugo.

Akizungumza baada ya kufungwa kwa maonesho hayo, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula amesema ushindi huo ni matokeo ya jitihada za Taasisi katika kubadilisha matokeo ya tafiti kuwa teknolojia na bunifu zinazoweza kutumika katika jamii na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Bidhaa bora zinahitaji utafiti. NM-AIST kama Taasisi inayotanguliza utafiti na ubunifu, imeendelea kuhakikisha matokeo ya tafiti yanabadilishwa kuwa teknolojia zinazotoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji,” amesema.

Amesema miongoni mwa teknolojia zilizooneshwa na NM-AIST katika maonesho hayo ni Mfumo wa Ng’ombe Smart, unaolenga kuongeza tija katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kuwezesha ufuatiliaji wa uzalishaji wa maziwa pamoja na taarifa muhimu za mifugo.

Aidha, amesema NM-AIST imewasilisha teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza thamani ya mazao, yakiwemo tumbaku na mazao ya chakula, pamoja na teknolojia zinazohusiana na uzalishaji wa vyakula vya mifugo kama kuku na ng’ombe.

Prof. Kipanyula amesema NM-AIST itaendelea kujipanga kuwa kinara katika kuchangia utekelezaji wa *Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050*, hususan kupitia utafiti na maendeleo, sayansi, teknolojia na ubunifu, pamoja na mabadiliko ya kidijitali.

“Ushindi huu ni chachu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi. Mwaka ujao tutakuja na teknolojia mpya kabisa. Mwaka huu tumefanikiwa kuzalisha takribani patent 40, jambo tunalojivunia na linalotupa nguvu ya kuendelea kuzalisha teknolojia na bunifu zenye tija kwa sekta ya kilimo na mifugo,” amesema.

Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini 2026 yamefungwa rasmi leo baada ya kushirikisha wadau mbalimbali katika sekta za kilimo, mifugo, elimu, utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu, ambapo NM-AIST imeendelea kuonesha nafasi yake katika kutumia utafiti na ubunifu kuchochea maendeleo ya jamii na sekta za uzalishaji.

Tags: